MWASENDA DEVELOPMENT INTERVENTION (MDI - NGO)

JIPATIE ZANA SABA (7) ZA KUJIFUNZIA LUGHA YA KIINGEREZA.

JIPATIE ZANA SABA (7) ZA KUJIFUNZIA LUGHA YA KIINGEREZA.

Kiingereza ni Lugha iliyosambaa zaidi duniani na inatumiwa na watu wa mataifa mbalimbali ukilinganisha na lugha nyingine kutokana na umuhimu wake katika mawasiliano, shughuli za kibiashara na taaluma.

Asili ya Lugha ya Kiingereza ipo nchini Uingereza tangu karne ya tano kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo (A.D) wakati Wajerumani walipohamia katika nchi hiyo ambapo mchanganyiko wa lugha zao na zile za wazawa kwa karne kadhaa zikapelekea kuundwa kwa lugha ya Kiingereza.

Utawala wa Uingereza ulipata fursa ya kusambaza lugha yao katika mataifa mbalimbali barani Amerika wakati wa enzi za utumwa, na Afrika na India katika zama za ukoloni.

Tofauti na Wakoloni wa Kijerumani waliopokonywa makoloni yao baada ya kushindwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, dola ya Uingereza iliweka jitihada za kufundisha Lugha ya Kiingereza kupitia mfumo rasmi wa elimu kwa wenyeji wa maeneo waliyoyatawala na pindi walipowapa uhuru waliacha mfumo unaosisitiza matumizi ya Kiingereza hadi sasa.

Mataifa yanayotumia lugha hiyo kama lugha ya kwanza ni pamoja na Uingereza, Marekani, Kanada, New Zealand na Australia wakati Mataifa mengine hujifunza Kiingereza kama Lugha ya kigeni au lugha ya pili.

Nchini Tanzania ambapo idadi kubwa ya wananchi wanaishi vijijini hujifunza Kiingereza kama lugha ya tatu ikitanguliwa na lugha za kikabila na Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya kufundishia ngazi ya elimu ya msingi katika shule za umma.

Kutokana na mtaala wa elimu nchini kuweka mkazo ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kuanzia ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu si jambo la kushangaza kuona mhitimu wa chuo kikuu anashindwa kujieleza kwa kutumia lugha hiyo hali inayopelekea kushindwa kumudu ushindani katika soko la ajira na mawasiliano kimataifa.

Miaka 15 ya elimu ya awali, msingi na sekondari haimjengei uwezo mwanafunzi kumudu matumizi ya lugha ya Kiingereza kwa ufasaha ingawa wengi hufaulu vizuri Mitihani ya Taifa na kujiunga na Elimu ya Juu kwa sababu ya mkazo uliowekwa katika mitaala ya elimu nchini na namna inavyotekelezwa unamlazimu mwanafunzi kukariri zaidi kwa hofu ya kufeli mitihani.

Kipindi kigumu katika maisha ya shule ni mwanzo wa elimu ya sekondari pale Lugha ya Kiingereza inapoanza kutumika kufundishia takribani masomo yote tofauti na shule za msingi ambako Kiingereza hufundishwa kama somo huku Kiswahili kikitumika kama Lugha ya kufundishia.

Lakini kilio hiki hakiwagusi wanafunzi waliosoma katika shule binafsi za msingi (English Medium Schools) zinazotumia lugha hiyo ‘ghali’ kufundishia na kujifunzia.

Ujuzi mdogo wa Lugha ya kufundishia miongoni mwa walimu unatajwa kama mojawapo ya vikwazo vinavyosababisha jamii kuhisi mtu anayemudu kuzungumza na kuandika lugha hiyo kwa ufasaha ana upeo mkubwa wa kiakili ukilinganisha na wale wenzangu na mimi.

Muelekeo huu wa kijamii unachangia kuminya fursa ya kujifunza lugha ya Kiingereza katika mazingira ya shule za umma kwa madhumuni ya kutumia ujuzi huo wa lugha kujiajiri, kuajiriwa na kujiendeleza kitaaluma kwa kutumia uwanja mpana wa mawasiliano na watu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mwalimu asiyemudu lugha ya kufundishia hawezi kufanikisha somo kwa sababu wanafunzi hawatopata nafasi ya kuuliza kwa undani kuhusu somo linalofundishwa kwa lugha ya Kiingereza kwa kuhofia kumkosoa mwalimu.

Aidha, mwalimu huyu ambaye anatokana na mfumo ule ule wa shule za umma kwenye msingi mbovu wa kujifunza lugha ya Kiingereza ndiye anafundisha watoto wenye matatizo ya lugha, idadi inayozidi uwiano wa mwalimu na wanafunzi darasani, vifaa duni na mazingira yanayokatisha tamaa na anatumia lugha ya Kiswahili kufundishia somo la Kiingereza.

Vilevile, uhaba wa walimu wenye ujuzi unaostahiki kufundisha somo la Kiingereza unapunguza uwezekano wa kuwa na wahitimu wanaokubalika kimataifa katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo japokuwa si ujuzi wa lugha pekee utampa sifa ya ubora mhitimu.

Utafiti unaonesha kwamba idadi kubwa ya walimu wa lugha ya Kiingereza hawatumii zana za kufundishia kama wanavyoelekezwa katika muhtasari wa somo hilo. Walimu wachache hujitolea kununua vifaa vya kufundishia kama magazeti lakini hata vile vifaa wanavyoweza kutengeneza hupatikana kwa uchache.

Matumizi ya vifaa vya mawasiliano vinavyotoa sauti na vile vinavyotoa sauti na picha, kwa mfano redio na luninga ni muhimu katika kufanikisha somo lakini inashindikana kutumika katika shule zisizo na miundombinu ya umeme hususani maeneo ya vijijini.

Ongezeko la familia zinazomiliki Luninga na fursa ya mwanafunzi kuangalia programu za luninga katika maeneo mengine tofauti na nyumbani bado hazijatatua changamoto ya kujifunza lugha ya Kiingereza nje ya taasisi za elimu kwa namna moja au nyingine kutokana na kukosa maelekezo ya namna ya kujifunza zaidi.

Lugha ya Kiingereza itaendelea kuonekana ni ghali na ya anasa miongoni mwa wanafunzi iwapo wanafunzi hawatojifunza kupitia majadiliano, tafiti, kusoma vitabu kwa lengo la kuongeza maarifa na kutumia lugha hiyo wakati wa masomo.

Kwa upande mwingine Sera ya Elimu na Mafunzo haijaweka mpango mkakati wa kuandaa walimu wa somo la Kiingereza, kuboresha mazingira na vifaa vya kufundishia na kujifunzia hivyo ni dhahiri changamoto ya kuwa na wasomi wasioweza kufanya mawasiliano kwa kutumia lugha ya Kiingereza itaendelea.

Katika bajeti miaka mingi hapa nchini  sekta ya elimu bado hutupwa katika kundi la pili kwa umuhimu jambo linaloashiria kwamba maendeleo ya elimu yatazidi kuwa changamoto kwetu.

Kwa kuwa Tanzania si kisiwa katika suala la maendeleo, ipo haja ya kuweka mikakati ya kuimarisha elimu ya msingi ambayo  hutolewa kwa muda wa miaka mingi, kwa kuandaa walimu wa somo la Kiingereza inavyopasa.

Mwalimu asiyemudu kutumia lugha ya Kiingereza katika mchakato wa kutoa elimu hawezi kumfundisha mwanafunzi kwa ufanisi na tukategemea kuwa na wahitimu wanaoweza kuunganisha taifa letu na mataifa mengine duniani kwa kutumia lugha ya Kingereza ambayo imesambaa zaidi na inatumika kama lugha ya kibiashara.

Haitoshi kuwa na walimu bora iwapo miundombinu ya madarasa, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na utayari wa wanafunzi hautokuwepo. Ili kukabiliana na tatizo hili tunahitaji nia dhabiti toka kwa wazazi wenyewe kwani kuendelea kuilalamikia serikali sio suruhisho.


Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi duniani ambazo zinatumia lugha tofauti na Kiingereza lakini zina wajibu wa kufundisha lugha mbalimbali za kigeni kutokana na umuhimu wake kuwezesha mawasiliano na nchi nyingine ili kuinua maendeleo.

Kwa kulitambua hilo, sisi Mwasenda Development Intervention (NGO) tunaendesha kampeini ya kutafuta zana za kufundishia na kujifunzia Kiingereza ili kuweza kuokoa jahazi litaloelekea kuzama. Tumeandaa zana saba (7) za kutatua tatizo hilo ambazo zinapatikana kwa soft copy na hard copy.

Kwa maelezo zaidi; karibu kituoni kwetu – Mwasenda Development Intervention – Nyasaka Centre (Nyamuge) jijini Mwanza – Tanzania.  Wasiliana nasi  kwa 0655-533543 au kwa barua pepe – mwasenda2018@gmail.com / info@mwasenda.org

Ahsante na Karibu Mwasenda

B. I. Kahuta.

Katibu Mtendaji – MDI

Leave a Reply