MWASENDA DEVELOPMENT INTERVENTION (MDI - NGO)

JITAMBUE CLUB

JITAMBUE CLUB

Nikushirikishe kwenye wazo muhimu  sana na lenye maana kubwa sana kwako. Si jingine  bali ni wazo la kuanzisha club ya JITAMBUE hapo ulipo; itakayoshughulika na utoaji wa elimu ya kujitambua kwa wanaclub.  Mipango yako  yote ya kiuchumi, kiafya, kiimani na kijamii haiwezi kufanikiwa iwapo utakuwa hujitambui. Changamoto tunazokutana nazo kwenye jamii ni kwa sababu wahusika wa changamoto hizo hawajitambui.

Hapa natoa mifano michache tu; kuna watu wanaishi mapolini na wanayafurahia maisha  hayo. Ni kwa sababu hawajawa na utambuzi wa kwamba kuna maisha mengine mazuri zaidi ya hayo. Hivyo hata wewe hata kama unayafurahia maisha au la! Ni kwa sababu hujatambua kuwa kuna maisha mengine mazuri tena ya ajabu zaidi ya haya unayoishi.

Jamii yetu kwa sasa iko kwenye vuguvugu la kupambana na umomonyokaji wa maadili; tunapambana na mashoga, machangu doa, wala rushwa, watumia dawa za kulevya, mafisadi, ujinga, maradhi, umaskini n.k. Hawa wote hawana elimu ya kujitambua ndiyo maana wametumbukia kwenye  mashimo hayo. Kijana  wa kiume anayetambua mwili wake vyema, akatambua matumizi ya kila kiungo alicho nacho, hawezi kutumika kinyume (mdomo wa kulia chakula utumike kingono?). Binti mrembo mwenye elimu yake anayetambua thamani ya mtoto wa kike hawezi kufanya biashara ya mwili wake. Mtumishi anayejua wajibu wake na kuthamini ya watu anaowahudumia hawezi kupokea rushwa. Mwananchi anayejua haki zake za msingi kwenye kupatiwa huduma hawezi kutoa rushwa. Kiongozi mwenye kujitambua na kujua wajibu wake kwa wadhifa alio nao hawezi kusaini mikataba yenye kuliangamiza taifa lake. Mwananchi anayetambua thamani yake hawezi kuhongwa chumvi na kofia ili kuiuza haki yake kwa kipindi cha miaka mitano. Binadamu yeyote mwenye kujua kuwa mwili ni nyumba ya Mungu hawezi kuiharibu nyumba hiyo – kwa kuondoa uhai wa mwenzie. Hiyo ni mifano michache tu ya matunda ya mtu kutokujitambua.

Kama jamii tumekuwa tukiangaika na matawi / majani ya changamoto badala ya kuhaika na mzizi. Kwa pamoja tuungane ili kuung’oa mzizi wa matatizo yanayoiadhiri jamii. Sehemu ya kuanzia kushughulika nayo ni watoto kuanzia miaka 5-14; kundi lililoko kwenye ngazi ya awali ya kupata elimu. Wajulishwe matumizi sahihi ya viungo vyao vya miili na wajue ni wapi pa kutoa taarifa pindi watakapofanyiwa vitendo tofauti na walivyofundishwa. Sehemu nyingine ya kushughulikia ni kundi la vijana wanaobarehe (14 – 22). Kundi hili likijitambua lina nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko ya kila sekta.

Kwa hayo machache, nakushauri wewe unayesoma hapa uanzishe club hapo ulipo ili uweze kuisaidia jamii yetu iweze kujitambua. Sisi  Mwasenda Development Intervention (MDI); kama shirika lisilo la kiserikali – NGO, tumeliona hilo na kuanza kulifanyia kazi. Tumeanza kwa kutoa kitabu chenye jina la JITAMBUE. Kitabu hicho kina kurasa 63, kinamsaidia msomaji kuweza kujua  yafuatayo:- yeye ni nani, maisha ni nini, kwa nini kafungwa kifikra,  mbinu za kujiamini, namna ya kubadili kawaida ya maisha yake, njia za kuiheshimu nafsi, zijue lawama usizostahili, namna ya kufanya maamuzi sahihi na mwisho ni njia za kusafisha ubongo.

Inusuru jamii yako kwa kuanzisha club za JITAMBUE, sisi MDI tutakuwa nawe bega kwa bega kwenye kukupatia machapisho mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha vuguvugu la mapinduzi ya kifikra.   Upatapo ujumbe huu tujulishe ili tukupatie mwongozo wa namna ya kufungua club ya JITAMBUE kwenye jamii yako.

Kauli mbiu:  “TUSIANGAIKE NA MATOKEO, BALI TUANGAIKIE MZIZI”

B. I. Kahuta

Katibu Mtendaji – MDI

This Post Has One Comment

  1. Hongera
    Tuzidi kushirikishana fursa ili hatimae jamii ipate elimu kombozi hususani vijana

Leave a Reply