MWASENDA DEVELOPMENT INTERVENTION (MDI - NGO)

TUSAIDIANE KUONDOA KUTU VICHWANI MWETU

TUSAIDIANE KUONDOA KUTU VICHWANI MWETU

Vijana wengi wa Tanzania tuna shida kubwa katika bongo zetu. Tumegeuka kuwa jamii ya kulaumu na kulalamika badala ya kuchukua hatua.Tunapenda urahisi. Tunasahau kuwa zama zimebadilika. Hatufikirishi vichwa vyetu kujaribu kutumia japo sehemu ndogo ya elimu tuliyoipata chuoni kutafuta fursa za kukamata.

Badala yake tumekaa tukibweteka tukiamini siku moja tutapata kazi ya ndoto zetu huku siku zikizidi kuyoyoma bila mafanikio. Tumekuwa mizigo kwa wazazi wetu badala ya kuwa msaada. Hakuna mawazo mapya tunayotoa. Zaidi tunatamani utanashati bila kuwa na pesa mfukoni. Kazi za kuchafuka hatuzitaki tena hata kama zinatengeneza pesa kiasi gani. Usomi wetu umetufanya tuchague kazi.

Kijana asiyeenda shule, unakuta ana uwezo mkubwa zaidi wa kutengeneza pesa, kuliko msomi aliyehitimu chuo kikuu. Kijana asiyefika chuo kikuu hachagui kazi na vilevile yuko tayari kumtumia msomi kuuliza kitu asichokijua, lakini msomi yeye kwa upande wake hayuko tayari kujifunza kutoka kwa kijana asiyebahatika kufika chuo kikuu.

Tuna tatizo kubwa sana. Vijana wengi tumekosa mawazo mapya ya Ujasiriamali. Bongo zetu zimelala. Hatuoni fursa mpya pamoja na kwamba fursa hizo zimejaa tele mtaani. Tunahitaji kufunguliwa vichwa vyetu na macho ili tuweza kuondolewa tongotongo zinazotufanya tushishindwe kuona fursa.

Changamoto ya kushindwa kuona fursa haiwakabili tu vijana wasomi waliyohitimu vyuo mbalimbali pekee yao bali hata wazee wetu waliyostaafu kutoka kwenye utumishi wa umma au sekta binafsi nao wanakabiliwa na tatizo hili.

Utastaajabu kumwona mstaafu namna anavyohangaika mtaani kuyakabili maisha yake mapya. Hawezi kufanya kazi nyingine zilizo nje ya fani yake. Matokeo yake baada ya kustaafu utumishi wake, anakuwa hana uwezo tena wa kuratibu na kusimamia mradi utakaompatia pesa na kumwezesha kuishi maisha yanayofanana na yale aliyokuwa akiyaishi alipokuwa kazini.

Mstaafu anaishi maisha ya ajabu kabisa pamoja na kwamba, alipatiwa mafao yake yote na mfuko wake wa hifadhi ya jamii. Amekosa elimu ya ujasiriamali. Pesa za mafao yake ya kustastaafu, anaingiza kwenye miradi mfu. Matokeo yake anapata anguko kubwa lisilo kuwa na mfano.

Lakini yote hii ni kwa sababu hakuna taasisi au watu waliyojitoa sawasawa kunoa bongo za watu wengine ili wawe na uwezo kujitegemea mara baada ya kustaafu au kumaliza viwango mbalimbali vya elimu.

Ipo haja ya kufundisha  stadi mbalimbali za kilimo biashara ikiwemo mbinu bora za kuendesha kilimo cha kisasa, kilimo chenye tija, ufugaji bora, Uongezaji wa thamani wa mazao ya Kilimo na mifugo, Usindikaji wa bidhaa mbalimbali za kilimo, uendeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuondoa tongotongo katika bongo za vijana, kuwawezesha vijana wahitimu wa vyuo kuwa na miradi yao binafsi na kupata fursa ya kusimamiwa kwa ukaribu na hatua kwa hatua hadi mradi utakaposimama.

Karibu MDI uelekezwe namna ya kijifunza.

Baika Kahuta

Executive Secretary – MDI

This Post Has 2 Comments

  1. Iko vzr lkn pia jaribuni kuwa mnaweka kwa lugha ya kingereza ili ipate uwanja mpana KTK kufikia watu wengi na kupata mawazo mchanganyiko kutoka sehemu tofauti.
    Mnajitahidi sana

  2. Noted with Thanks

Leave a Reply